STAA WA MUZIKI TEKNO ATANGAZA KUACHA BANGI

Staa wa muziki wa Afro-Beat wa Nigeria, Tekno Miles amewashangaza wengi baada ya kusema kwamba ameamua kuacha kabisa matumizi ya bangi au cha Arusha.

Kupitia video, Tekno anasema kuwa alifikia uamuzi huo na hadi juzi alikuwa tayari amemaliza zaidi ya saa 48 sawa na siku mbili bila kutumia msuba.

Tekno anasema kuwa, awali hangeweza kukaa bila kutumia bangi hata usiku mmoja, lakini sasa hata yeye haamini kama kweli ameweza kukaa zaidi ya saa 48 pasi na kukaribia bangi.

“Huyu ni mimi, saa 48 baadaye au tuseme zaidi ya saa hizo, bila bangi, bila marijuana, ninapenda jinsi ninavyoendelea nilipata japo kulala kiasi usiku. Ndiyo huyu mimi niko vizuri, macho yangu sasa yako vizuri hayana zile dalili za kuonesha utumizi wa vileo. Najua itakuwa vizuri hata zaidi,” anasema Tekno aliyetikisa vilivyo na Ngoma ya Pana.

Tekno si msanii wa kwanza kuweka wazi kuwa amekuwa akitumia dawa za kulevya ili kumpa mihemko ya kutinga studioni na kufanya ngoma ambazo aghalabu huwa na mapokezi makubwa kwa mashabiki wake.

Tekno kwa sasa anatamba na ngoma yake mpya ya After Party baada ya kuvuma vilivyo na kolabo ya Buga aliyoshirikishwa na Kizz Daniel.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post